|
Waafrika Waliojitoa Muhanga Karbala
Mwandishi:
Ra’isu’l Muballighin Allamah Al-Haj Sayyid
Saeed Akhtar Rizvi R.A.
Mfasiri:
Al-Haj J. J. Kiambu
Ni mara nyingine tena imewadia Siku ya Ashura mwezi 10 Muharram, pia ni
wakati mwingine Uislamu unapata nguvu kutokana na msukumo wa tukio la
masaibu ya Karbala; na hii ni indhari na ni kumbukumbu kwa matendo ya
kishujaa yaliyofanywa na Wana wa Afrika ambao waliandika ujumbe wa
(Haki) kweli kwa damu yao katika ardhi ya Karbala.
Uislamu, pamoja na Ujumbe wake kwa Walimwengu wote, tangu hapo awali
ulimpa Uhuru mwanadamu kutoka katika himaya ya Wadhalimu. Ilikuwa suala
lisilozuilika kwamba kilio cha “Hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa
Allah” kingeunganisha watu wa Mataifa yote na wa Imani mbalimbali.
Pamoja na ujumbe wake wa kujikomboa mwanadamu kiroho, Qur’an Tukufu
imewalingania binadamu kuungana pamoja bila ya kujali rangi wala utaifa
wao.
“Hapana shaka mbora wenu mbele ya Allah (s.w.t.) ni yule mwenye kumcha
Mwenyezi Mungu (Qur’an, 49:13). Ni kwa aya hii Mwenyezi Mungu
amempa mwanadamu Haki ya Uhuru wake. Wenye kufuzu na kulipwa mema (Pepo)
ni wale tu watakaotii amri zake bila kujali utaifa wao wala utukufu na
ubora wa makabila yao.
Kabla ya kuorodhesha majina ya Waafrika waliojitoa muhanga nafsi zao
huko katika ardhi ya Karbala ningependa kueleza kuwa hiyo haikuwa mara
ya kwanza kwa damu ya Waafrika kumwagika katika maidani ya kutetea Haki.
Ni ukweli usiopingika kuwa Mashahidi wa kwanza walikuwa Mwanamke
Mwafrika, Sumaiyya na mumewe, Yasir. Wao walikuwa watu wa kwanza kufa
mashahidi kwa kujitoa muhanga pale makafiri walipoishambulia Makka na
kuwaua kikatili.
Mtoto wao Ammar, alikuwa miongoni mwa maswahaba wa Mtukufu Mtume
(s.a.w.w.), mtu ambaye aliaminiwa sana na Mtume. Siku moja Mtume
(s.a.w.w.) alisema:
“Ammar, utauliwa na kikundi cha Makafiri. Wewe utakuwa unawaita wao
kwenye Pepo (Janah) na wao watakuwa wanakuita kuingia katika moto wa
Jahanamu. Ujumbe huu ulikamilika katika vita vya Siffini, wakati Ammar
alipopigana bega kwa bega upande wa Imamu Ali (a.s.) na kuuliwa na jeshi
la Moawiyya. Khabbab bin Al-Arrat alikuwa sahaba mwingine maarufu zama
za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza
kusilimu. Naye pia alitokea katika bara la Afrika, na aliuliwa na
makafiri walipoishambulia Makka wakati akipigania Haki.
Huko katika ardhi ya Karbala pia, ili kuendeleza jadi ya kujitoa
Muhanga, Afrika ilitoa mchango mkubwa kuutetea Uislamu. Tunapowakumbuka
Mashahidi waliouliwa Kerbaba wapatao 72, na 12 kati yao ni kutoka katika
Bara letu, kwa kweli tunafarjika kuona Afrika ilivyokuwa mstari wa mbele
kuinusuru Dini ya Allah (s.w.t.).
Katika siku hiyo ya msiba jeshi la maadui liliwashambulia Waislamu
alfajiri mapema. Jeshi la maadui lilikusudia kuwakanyaga kanyaga kwa
kwato za farasi maswahaba wote wa Imam Husein (a.s.), pamoja na familia
yake na watoto wadogo. (Idadi ya Wanaume, wanawake na watoto katika
msafara wa Imam Husein (a.s.) haikuwa zaidi ya watu 100). Lakini
maswahaba watiifu wa Imamu walijipanga vema na kusonga mbele. Jeshi la
Moawiyya lilikuwa na watu (makafiri) wapatao 4,000. Mapigano makali
yalianza na baada ya muda maadui walirudi nyuma. Kwa Imamu Husein (a.s.)
haukuwa ushindi mzuri, kwa kuwa aliwapoteza miongoni mwa marafiki zake
watiifu wapatao 50.
Miongoni mwa hao Mashujaa 50 walikuwepo Waafrika saba: Salim, Zahir,
Quarib bin Abdulla, Munjeh bin Salim, Saad bin al-Harth, Nasr bin Abi
Naizer na Harth bin Nab-han. Majina yao hawa mashahidi (Mashujaa)
yamewekwa katika kumbukumbu sio tu na Wanahistoria mashuhuri, bali pia
na Maimamu wetu walioandika Ziyarah wakiwataja Mashahidi wote mmoja
baada ya mwingine.
Shaudhab, Mwafrika mwingine alikuwa Mwanazuoni maarufu wa Shariah za
Kiislamu na Hadith wa wakati huo. Watu walikuwa wakisafiri masafa marefu
kuja kusikiliza hekima na nasaha zake. Baada ya kusikia ukweli wa Imamu
Husein (a.s.), Shaudhab pamoja na rafiki yake, Abis Shakiri, waliungana
na Imamu Husein (a.s.) na wakafa Mashahidi katika ardhi ya Karbala kwa
ajili ya kuunusuru Uislamu.
John; ambaye bila shaka alikuwa Mkristo aliyesilimu alikuwa Mtumwa wa
Kihabeshi ambaye baada ya kufariki “Bwana” wake; alichukuliwa na
familia ya Mtume ili aishi nao kama mgeni wao. Alibakia hapo kwa furaha
na amani kwa muda wa miaka 30 hivi. Aliungana na Imamu Husein kwenda
Karbala, ingawa alikuwa tayari ni mzee wakati huo lakini alipigana kwa
nguvu zake zote kabla ya kuuawa. Alipoanguka chini, Imam Husein
alimwendea, na akakinyanyua kichwa chake na kukilaza juu ya paja lake na
kumuombea.
Hadith za Kishia zinaelezea kuwa watu wa kabila la Asad waliokuja
kuwazika Mashahidi (Mashujaa) baada ya siku tatu walishangaa kuona mwili
wa marehemu unang’ara na unanukia kwa manukato mazuri ya peponi. Ulikuwa
mwili wa Shujaa, John.
Aquaba, pia kutoka Bara la Afrika alikuwa miongoni mwa maswahaba
waaminifu wa Imam Husein (a.s.). Imam aliacha nyaraka zake zote muhimu
chini ya uangalizi wa Aquaba. Alijeruhiwa katika vita vya Karbala, na
alichukuliwa mateka pamoja na familia ya Imam. Akiwa miongoni mwa watu
walioshuhudia mauwaji ya Karbala, amebaki kuwa kumbukumbu na kielelezo
muhimu katika Historia.
Miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Imamu Husein (a.s.) Karbala ni
mwanamke Mwafrika, Fizza (s.a.); ambaye atakumbukwa milele kutokana na
Imani yake na huduma zake kwa familia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Nchi
yake ya asili ilikuwa Nuba, ambayo hivi sasa ni Sudani. Kwanza alitoa
huduma kwa Bi. Fatima bint yake Mtume. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipanga
utaratibu kwamba siku moja Bi Fatima (a.s.) afanye kazi za nyumbani zote
na Fizza apumzike na siku ifuatayo Fizza afanye kazi hizo na Bi. Fatima
(a.s.) apumzike.
Baada ya kufariki dunia Bi. Fatima (a.s.), Fizza (s.a.) aliolewa na
Muislamu mcha Mungu na akaweza kuitunza familia yake, lakini uwajibikaji
wake kwenye nyumba ya Imamu Ali (a.s.) uliendelea kama kawaida.
Aliungana na Imam Husain kwenda Karbala na kuwa pamoja nao katika
madhila, maafa na masaibu yaliyowapata wanawake na watoto wa Imam katika
ardhiya Karbala.
Elimu ya Qur’an ya Fizza (s.a.), imeelezewa na Mwanazuoni maarufu Abul
Qasim Qushairi. Mwanazuoni huyu ameandika katika wasifu wa Fizza kwamba,
kwenye miaka 20 ya mwisho ya uhai wake Fizza hakuweza kutamka neno lake
mwenyewe, wakati wote alizungumza au kusoma aya kutoka katika Kitabu
Kitakatifu Qur`an.
Uislamu unajivunia watoto wa ardhi ya Afrika ambao kwa mapenzi yao
walijitolea muhanga kuinusuru Dini ya Allah (s.w.t.). Kizazi cha Imam
Husain (a.s.) wakati wote walitoa heshima zao kwa Mashahidi wa Karbala
kwa maneno yafuatayo:-
“Heshima juu yenu Enyi mlioridhiwa na Allah pamoja na Waja Wake. Heshima
juu yenu Enyi Wasaidizi wa Imani. Naomba Wazazi wangu wapate Heshima ya
kuyaweka Maisha yao kwa ajili yenu. Mlikuwa Watakatifu na Watoharifu na
mpo watakatifu na Watoharifu hapo mlipo milele. Kwa hali ya juu mmefuzu,
Ninamuomba Allah aniweke pamoja nanyi ili niwe miongoni mwa wenye
kufuzu.”
|