UTUKUFU WA IMAM HUSSEIN BIN ALI BIN ABI TALIB (A.S.)

Kimeandikwa Na: Sayyid Murtaza Rizvi

 

Imamu Hussein ni katika wale ambao Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatoharisha na kuwatakasa na machafu kama ilivyo katika Qur’ani Tukufu Sura ya 33:33. Imepokewa kutoka kwa Ummu-Salama (mke wa Mtume) kwamba  ilipoteremka Aya hii ya utakaso (33:33) ndani ya nyumba yangu, nikiwa mlangoni pamoja na Mtume na Ali, Fatimah, Hassan na Hussein pamoja na Malaika Jibril na Mikail wakiwa ndani ya nyumba yangu, nilisema:-

 

“Ewe Mtume! Je! Mimi si katika Ahlul –Bayt wako?.  Mtume (s.a.w.w.) akasema,”  Hakika wewe Ummu Salama u katika kheri na wewe ni katika wake za Mtume (s.a.w.w.). Rejea: (Durrul Manthur- Juzuu ya 6, Uk. 604-605. na Tafsiri Tabari Juzuu ya 10, Uk. 298 na Tafsiri Ibn Kathir Juzuu ya 3, Uk. 531).

 

Iliposhuka Aya ya Mawaddatul-Kurba (Sura ya 42:23), Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume (s.a.w.w.) katika Qur’an tukufu awaambie Ummah wake hivi:- “Qul laa as-alukum alayhi ajran il-lal Mawaddata fil-Qurbaa” waambie siwataki malipo yoyote juu ya (Utume niliokuja nao) ila mapenzi juu ya Aqraba wangu (42:23).   Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa, hawa Mawaddatul-fil Kurba (Aqraba) ni nani na akajibu ni watu wa nyumba yake yaani Ahlul-Bayt. Aya hii inaweka wazi kuwa kuwapenda Ahlu-Bayt wa Mtume ni wajibu usio shaka juu ya kila Muislamu. Rejea: (Tafsiri Ibn Kathir Juzuu ya 4, Uk. 121-123. na Fathul Qadiir Juzuu ya 4, Uk. 760. na Tafsiri Tabari Juzuu ya 11, Uk. 142-145. na Durrul Manthur- Juzuu ya 7, Uk. 348-349.).

     

Ilipoteremshwa Aya ya kuapizana yaani “Mubahala” alipoambiwa Mtume (s.a.w.w.) Sema; Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu na wake zetu na wake zenu na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuapizane. Mtume alitoka na Sayyidna Imam Hassan na Imam Hussein (watoto wake) Bibi Fatima (mke wa Imam Ali bin Abi Talib), Mtume (s.a.w.w.) na Sayyidna Imam Ali (Nafsi zetu).  Makafiri wa Najran walipomuona Mtume (s.a.w.w.) na nyuso za wale watukufu na watoharifu Ahlul-Bayt wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) walikataa kuapizana na badala yake walikubali kulipa jizya (kodi). Rejea: (Ruhul-Maan J. 2   Uk. 180-181. na Fadhul-Qadiyr J. 11 Uk. 524. na Durrul- Manthur J. 2   Uk. 232-233.).

 

Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Ewe Mola! Mimi nampenda Hussein nawe mpende, Hussein anatokana na mimi na mimi ninatokana na Hussein, umpende mwenye kumpenda (Hussein)”. Rejea: (Sahih Muslim J. 4   Uk. 1293.). Na vile vile Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Hasan na Hussein ni mabwana wa vijana wa Peponi, anipendae awapende hawa wawili”. Rejea: (Sawaiqul Muhriqa Uk. 522.).

 

Kuwasalia Aali Muhammad ni nguzo ya Sala na kuacha kuwasalia wao ni kuibatilisha Sala. Rejea: (Sawaiqul Muhriqa Uk. 147.).

 

Pia amesema Bwana Mtume (s.a.w.w.): “Hakika Mfano wa Ahlul Bayt wangu kwenu ni mfano wa Safina ya Nabii Nuh (a.s.) waliopanda  Safina hiyo waliokoka na wale waliokataa kupanda Safina hiyo waliangamia.” Rejea: (Sawaiqul Muhriqa Uk. 150.).

 

Na mwisho ni kauli ya Imam Shafi aliposema: “Ikiwa dhambi yangu ni kuwapenda watoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) [Imam Hassan na Imam Hussein] basi ni dhambi ambazo sitatubia”.

 
 

Prepared by: Khoja Shia Ithna Asheri Dar es Salaam Juloos Committee 1429AH (2008)
Email us your comments, suggestions, articles, etc through the Website Coordinator: Murtaza H. Lalji