Tarehe 10 Muharram (Ashura)

Kimeandikwa Na: Sayyid Murtaza Rizvi

 

Imam Hussein (a.s.) na watu wake wenye kumcha Mungu walipigana kishujaa, kuulinda Uislam na kuitetea “La ilaha Illa llah” hadi tone lao la mwisho la damu.  Wasia aliouandika Imam Hussein (a.s.) alipokua akiondoka Madina ni “Mimi siondoki hapa Madina kwa sababu ya jeuri au kidunia bali nafuata njia ya babu yangu Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.) na njia ya baba yangu Imam Ali (a.s.) ya kuamrisha mema na kukataza maovu”.

 

Hatimaye Imam Hussein (a.s.) na watu wake walizingirwa Karbala na kunyimwa maji kwa siku 3.  Tarehe 10 Muharram ni siku ya Ashura ni siku kubwa ya huzuni, tukiwakumbuka Mashujaa hawa 72 wakiwemo mzee wa miaka 85 hadi mtoto mchanga wa miezi sita, wakiwemo waafrika, kwa ushujaa mkubwa waliouonyesha kwa kulinda Dini dhidi ya majeshi ya kidhalim yenye watu 32,000.

 

Imam Hussein (a.s.) na watu wake waliuwawa pamoja na mwanawe wa miezi sita.  Jeshi la Yazidi halikuridhika bali walichoma moto mahema ya wanawake watukufu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) na kuchukuliwa Syiria kama mateka wa vitani.

 

Qur’an tukufu inasema Mbingu na Ardhi hazikuwalilia watu waovu na wala hawakupewa muda wa kurejea Duniani.  Dhukhan 29 Aya  hii inaonyesha kwamba Mbingu na Ardhi haziwalilii watu waovu bali huwalilia watu wema kama ilivyopokewa na Sahaba Yazid Ibn Abi Ziyad aliposema: “Alipouliwa Imam Hussein (a.s.) Mbingu zilipiga wekundu kwa muda wa miezi minne na kusema kuwa wekundu wake ndio kulia kwake.” Rejea: (Tafsir Ibn Kathir J.  4, Uk. 155. na Duurul Manthur J. 7 Uk. 412 – 413.).

 

Msimamo wa Imam Hussein (a.s.) ungali hai na mhanga aliojitolea umo ndani ya nyoyo za Waumini ulimwenguni kote.  Haya ni malipo ya watu hawa kwa Mtume wao aliyeleta Dini na Ustaarabu.  Jazaa yao ni kuwaua wajukuu zake.  Wameipinga Qur’ani (42:23) isemayo “waambie siwataki  malipo yoyote juu ya (Utume niliokuja nao) ila mapenzi juu ya Aqraba wangu.”

 

Tumempenda Mtume (s.a.w.w.) basi lazima tuwapende anaowapenda yeye sio kuwaua.  Na mwisho Mtume (s.a.w.w.) aliusia:-  Mimi nawaachia nyinyi makhalifa wawili:  Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na watu wa nyumba yangu, na kwamba mkishikamana navyo kamwe hamtapotea baada yangu. Rejea: (Musnadi Ahmad J. 5, Uk. 189.).

 
 

Prepared by: Khoja Shia Ithna Asheri Dar es Salaam Juloos Committee 1429AH (2008)
Email us your comments, suggestions, articles, etc through the Website Coordinator: Murtaza H. Lalji