|
SAUMU YA ASHURA
JE KUFUNGA SIKU YA ASHURA NI SAWA ?
Mwandishi:
Ra’isul Mubalighin
Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi R.A.
Mutarjuma:
Amiraly M. H. Datoo
Baadhi ya Hadithi zinapatikana katika vitabu vya Ahl as-Sunnah
zinazosema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuhama kwenda
Madina, aliwakuta Mayahudi wakifunga (saumu), mwezi 10 Muharram
(Mfunguo nne). Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwauliza sababu ya kufanya
hivyo, alijibiwa: “Ni siku njema, siku ambayo Mungu aliwaokoa wana wa
Israil kutoka kwa adui yao (yaani Firauni); hivyo Mtume Musa alifunga
(saumu) siku hiyo.” Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mimi nastahiki zaidi kwa
Musa kuliko ninyi.”
Hivyo Mtume (s.a.w.w.) alifunga siku hiyo na kuwaamrisha Waislamu
wafunge siku hiyo. Rejea: Al-Sahih ya al-Bukhari, J. 3; chapa ya
Misri, uk. 54. na Mishkatul-Masabih, chapa ya Delhi; 1307 A.H.,
uk. 172.
Immetolewa maelezo na mfasiri wa Mishkatul-Masbih kwamba:
“Ilikuwa katika mwaka wa pili, kwa sababu katika mwaka wa kwanza Mtume
aliwasili Madina baada ya Ashura katika mwezi wa Rabiul-Awwal (mfunguo
sita).
Ni kiasi gani ilifikiriwa kuwa na umuhimu hivyo? Hiyo inaweza kuamuliwa
na Hadithi nyingine iliyosimuliwa katika al-Sahih al-Bukhari:
“Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha mtu mmoja kutoka kabila la Aslam:
‘Watangazie watu kwamba yeyote ambaye amekula chochote, basi afunge
sehemu ya siku iliyobakia, na yeyote yule ambaye hajala, basi afunge
siku hiyo nzima, kwani leo ni siku ya Ashura (mwezi 10
Muharram)’”
Ni katika mwaka huo ambapo saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
iliwajibishwa, na wajibu wa kufunga siku ya Ashura ukaondolewa,
kama ambavyo imedaiwa katiaka Hadthi nyingine zilizosimuliwa katika
kitabu hicho hicho. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, bado
inapewa umuhimu mkubwa kama saumu ya Sunnah!!
Sasa hebu tuziangalie kwa ukaribu sana Hadithi hizi:
Kwanza: Mayahudi walikuwa na kalenda yao na miezi yao. Hakuna mantiki
yoyote kwamba walikuwa wakifunga siku ya Ashura mwezi 10 Muharram
- mpaka ithibitishwe kwamba tarehe hii siku zote inawiana na siku ya
Mayahudi ya kufunga.
Imetajwa katika makala yangu ya, “Matryrdom of Imam Husayn and the
Muslim and the Jewish Calendars” (Alserat, vol. VI. No’s 3 & 4; Muharram
1401 Nov. 1980) kwamba mwezi wa kwanza wa Mayahudi (Abib
baadae ukaitwa Nisan) ulikuwa ukifungana na mwezi wa Rajabu
wa Waarabu. W. O. E. Oesterley na Theodore H. Robinson
wameandika kwamba katika Arabia “sherehe muhimu zaidi kuliko zote ni ile
ambayo huangukia katika mwezi wa Rajabu (sic), sawa na mwezi wa Kiyahudi
Abib, kwani huu ulikuwa wakati ambao Waarabu wanasherehekea
majira ya kuchipua baada ya kipupwe.” (Hebrew Religion; S.P.C.K.,
London; 1955; uk. 128)
Yumkini, katika zama za kale za matawi mawili ya nyumba ya Ibrahim
walifuata mfumo huu huu wa kuongheza siku (intercalating),
nyongeza ya mwezi mara saba katika mzunguuko wa mika 19. Na katika njia
hii mwezi wa saba wa Mayahudi, Tishri I, ulifungana na
Muharram. Na Ashura ya Muharram ililingana na mwezi 10 ya Tishri I,
siku ya Mayahudi ya upatanisho - siku ya kufunga.
Katika makala hiyo ilielezwa kwamba kalenda hizo mbili zimepoteza uwiano
wake wakati katika karne ya 9 hijra Uislamu ulipokataza uongezaji wa
siku katika mwaka (intercalation). Lakini katika kuchunguza kwa
kina inaonekana kwamba kulingana huko kulipotea zamani zaidi kabla ya
kuja kwa Uislamu, kwa sababu Waraabu hawakufuata mpango wowote wa
kihesabu katika uongezaji wao wa siku (intercalation).
Hii ndio maana Muharram ya mwaka wa pili Hijra ulianza tarehe 5 Julai,
623 C.E. (Al-Munjid, chapisho la 21), miezi kabla ya Tishri I
(ambao kila siku unafungana na Septemba - Oktoba).
Kwa uwazi, Ashura ya Muharram katika mwaka huo (au,
ilivyo, wakati wa uhai wote wa Mtume kule Madina) haikuwa na umuhimu
wowote ule uwao kwa ajili ya Mayahudi.
Swali ni: Kwa nini walifunga katika siku hiyo?
Pili: Maandiko ya Kiyahudi ya Midrashic huelezea siku ya 10 ya
mwezi wa 7 (Yom Hakippurim - Siku ya Upatanisho) kwenye tukio la
kurudisha Mbao za Agano kutoka Mlima Sinai, kama Dr. Mishael
Maswari-Caspi alivyoandika katika barua yake, iliyonukuliwa katika
makala yangu ya nyuma iliyotajwa hapo juu.
Swali ni: Kama Mayahudi walitaka kuweka mawiano ya muda mrefu
yaliyopotea ya Tishri na Muharram katika mazingatio, imekuaje
kwamba wamesahau kuisimulia Hadithi hii kwa Mtume?
Tatu: Mwezi ambao Mungu aliwakomboa Mayahudi kutoka kwa Firauni ilikuwa
ni Abib (yaani, Rajabu), kama Biblia inavyosema kwa uwazi: (Deut. 16: 1)
Swali ni: Inawezekanaje kwa Mayahudi kuhamisha tukio la Abib (kwa
asili hufungana na mwezi wa Rajabu) kwenda Muharram, kwa kuiasi
Taurati wazi wazi?
Na mwisho, hapa kuna nukta ya kutafakari kwa Waislamu: Mtume Muhammad
(s.a.w.w.) alitumwa pamoja na dini ili azifute dini zote na shari’ah
zote zilizokuja nyuma yake. Ni vipi kwamba anaridhia au kujidhili kuiga
desturi na mila za Mayahudi?
Ni wazi kutokana na ukweli uliotajwa hapo juu, kwamba Mayahudi walikuwa
hawana sababu yoyote ya kufunga katika siku ya Ashura ya Muharram
katika wakati huo; na kisa hiki, kilichojengwa juu ya kigezo hicho, ni
habari za kubuni tu. Kwa hakika zilibuniwa na msimuliaji (wa Hadithi)
ambaye alijua tu kwamba hapo zamani za kale Muharram ilifungana na mwezi
wa Tishri I; lakini alikuwa haelewi kabisa dini ya Wayahudi ya
wakati ule ule na utamaduni.
Mtu hujiona amelazimika hapa kutaja kwamba Hadithi hii na nyingine kama
hii zilibuniwa na kambi ya wafuasi wa Bani Umayyah, baada ya
muhanga wa Imamu Huseini (a.s.), kama sehemu ya kampeini yao ya kuigeuza
siku ya Ashura, mwezi 10 Muharram kuwa siku ya
kusheherekea.
Hadithi hizi ni za aina moja kama zile zinzosema kwamba mwezi 10
Muharram Safina ya Nuh ilisimama juu ya Mlima wa Arafat, moto
ulikuwa baridi na salama juu ya Ibrahim, na Isa (Yesu) alipaa kwenda
mbinguni.
Katika kundi hilo hilo zimekuja Hadithi zenye kuwahimiza Waisalmu
kuifanya Ashura siku ya shangwe ya siku kuu, na mtu kuweka hakiba
ya nafaka (chakula) mahususi kwa ajili ya siku hii kwa vile itaongeza
riziki ya mtu na kuleta baraka za Allah kwa watu wa kaya (familia).
|