|
HOTUBA YA AL-USTADH SHEIKH ABDULLAH IBN SALEH AL-FARSI ALIYOITOA KWENYE
HAFLA YA KUKUMBUKA YA MAUAJI YA IMAM HUSAIN BIN ALI (A.S) -
ZANZIBAR 1361 A.H 1942 A.D
Enyi wageni waheshimiwa na nyote mliohudhuria.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu. Sifa zote
njema anastahiki kusifiwa Mwenyezi Mungu Mola wa waliomwengu. Kisha sala
na salamu zimshukie mbora wa Mitume na Manabii, Bwana wetu Muhammad
aliyemuaminifu na pia ziwashukie kizazi chake ambao Mwenyezi
amewaondolea uchafu na kuwatakasa mno.
Ama baada, kwa hakika kamati iliyoandaa kumbukumbu hii ya mauaji ya Imam
Husain a.s ilikuwa imemtaka mwalimu wangu Al-Allamah Sheikh Abubakar Ibn
Abdillah Bakathir aje asimame kwenye mahafali hii tukufu ili azungumzie
japo kidogo tu kuhusu tukio hili kubwa lililotokea Karbala. Tukio
ambalo hapana shaka japo nila siku nyingi lakini haliwi kongwe wala
uchungu wake hausahauliki pamoja na kupitiwa na miezi mingi na miaka
mingi.
Kwa kuwa siku hizi afya ya Sheikh siyo nzuri ameniteuwa nimuwakilishe
mahala hapa japo kuwa mimi si miongoni mwa watu wa rika lake wala siko
kati ya watu wenye ufasaha wa kiwango chake.
Hapana shaka kwamba yeye alikuwa ndiyo mwenye kustahiki mno mahala hapa,
lakini maamuzi ya Mwenyezi Mungu ndiyo yenye kupita pindi yanapo mfika
mtu basi huwa hana njia ya kuyaepuka.
Na ilivyokuwa kuna mawaidha na mazingatio katika kumbukumbu za misiba,
tumeona ni vema tueleze mawaidha na mazingatio yaliyomo ndani ya msiba
huu mkubwa uliotukusanya katika usiku huu ili tuuhuishe.
Kwa hiyo mimi nasema kwamba, "Kwa hakika mauaji ya Imam Husain a.s ni
miongoni mwa matukio makuwa yenye kusikitisha na kuhuzunisha, lakini
makumbusho yake ni yenye manufaa japokuwa hadithi yake inamtia huzuni
kila Muislamu na kumchukiza kila mwenye akili."
Huenda Mtu asiye jua kitu kuhusu mwenendo wa Mwenyezi Mungu kwa ujumbe
wake akasema, "Ni kwa nini basi Mwenyezi Mungu hawasaidii watu wa haki
dhidi ya maadui wao ambao wako kwenye upotovu bila hata ya wao kunyanyua
panga zao (dhidi ya madui hao) wala bila mapambano ya mikuki?"
Sisi tutamjibu kwa kusema kuwa,"Hatuna shaka yoyote ndani ya nyoyo zetu
kwamba, Mwenyezi Mungu hawasaidii watu hao wa haki bila mapambano ili tu
apate kuwapambanua wale walioamini na wengine awafanye kuwa ni Mashahidi
miongoni mwao, kama alivyosema Mwenyezi Mungu ndani ya Sura Al-Imran,
"Ili Mwenyezi Mungu apambanuwe wale walioamini na awafanye miongoni
mwao kuwa ni mashahidi na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu, na ili
Mwenyezi Mungu awasafishe walioamini na kuwafuta waliokufuru" Na vile
vile aliposema ndani ya Suratul Baqarah, "Mnadhani kuwa mtaingia peponi
na hali hamjajiwa na mifano (wa yale yaliyowajia) wale waliopita kabla
yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa mno hata Mtume na
wale walioamini pamoja naye wakasema, "Msaada wa Mwenyezi Mungu utafika
lini? Jueni kuwa msaada wa Mwenyezi Mungu uko karibu." 2:214
Mawaidha na mazingatio yanayotokana na mauaji ya Imam Husain (a.s)
Hapana shaka kwamba hapo kabla nilikuahidini kwamba, nitakuelezeni
baadhi ya mawaidha na mazingatio yaliyomo ndani ya tukio la mauaji ya
Imam Husain a.s, kwa hiyo sasa hivi nitawaeleza kile nilichokuwa
nimekiahidi kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na ninasema:
Kwanza: Imam Husain a.s ndiyo mtu wa kwanza aliyeuonesha Umma njia ya
kutoka dhidi ya watawala waovu na wajeuri na akaulingania (Umma) kupinga
dhulma kwa kila mwenye uwezo wa kulifanya hilo. Hivyo basi aliitoa nafsi
yake na akajitolea damu yake ili kusimamisha haki, uadilifu na Sunna ya
Mtume s.a.w dhidi ya maovu, ubinafsi na kulewa madaraka.
Hapana shaka kwamba babu yake s.a.w amesema, "Yeyote atakayeanzisha
mwenendo mzuri basi atapata ujira wake na ujira wa wale watakaoutumia
mwenendo huo” Nampa hongera Imam huyu kwa kuweka mwenendo huu mzuri.
Pili: kitendo hicho cha Imam Husain a.s kilikuwa ni cha kuwatia nguvu na
kuwapa moyo wa kujituma wale wote ambao wanapata matatizo katika
kutumikia dini ya Mwenyezi Mungu ili wasije wakajiona kuwa pengine
wanapatwa na matatizo hayo kwa sababu labda wao ni wanyonge na ni watu
dhalili mbele ya Mwenyezi Mungu, au labda wakahisi kuwa wao wako kwenye
batili na maadui zao ndiyo walio kwenye haki kwa hayo wayatendayo, na
kwa ajili hii wakavunjika nguvu na kuacha msimamo wao. Lakini iwapo tu
watamkumbuka Imam Husain a.s. na misiba iliyompata hali ya kuwa yeye
alikuwa akitetea haki na maadui zake wakitetea batili, basi hapo watu
wema hujirudi kutokana na dhana ile potofu, kwani watu wengi hufikia
hali aliyoisema MwenyeziMungu katika Suratul-ankabut. "Na miongoni mwao
wako wanaosema, tumemwamini Mwenyezi Mungu, lakini wanapoudhiwa katika
njia ya Mwenyezi Mungu huvifanya vituko vile vinavyowakuta toka kwa watu
kama kwamba ni adhabu ya Mwenyezi Mungu."
Tatu: Tukio la kujitoa Muhanga Imam Husain a.s liwe ni mazingatio kwa
yeyote yule atakayesongwa na matatizo ya ulimwengu yanayotokana na
dhulma kiasi cha yeye aone kuwa anawajibika kufa kuliko kuendelea
kuishi. Na Imam Husain ni mtu Mtukufu mno katika zama zake wala hana
mfano popote duniani, kwa sababu nafsi yake tukufu ilikataa dhulma na
unyonge akachagua kifo kuliko udhalili, na akawa kama alivyosema Ibn
Nubatah, "Na Husain ndiye yule ambaye aliyaona mauti kuwa ni jambo
tukufu katika maisha, na kuishi katika udhalili ni sawa na kifo."
Nne: Husain a.s awe ni mtu wa kupigia mfano kutokana na ushujaa wake,
uhodari wa msimamo wake, kutokana na tofauti kubwa iliyokuwa baina ya
kikundi chake na jeshi la adui yake ambalo lilikuwa kubwa mno kwa idadi
na maandalizi, kiasi ambacho sicha kulinganisha. Basi yafaa jambo hilo
liwe la mazingatio kwa mwenye kuzingatia.
Tano: Imam Husain a.s pamoja na wote alikuwa nao miongoni mwa watu wa
nyumba yake wote wawe ni kitambulisho cha mashujaa na kiigizo chema
katika uvumilivu na ukarimu.
Sita: Athari ya Jihadi yake ibakie milele na mahali popote watu
watakapokuwa wanagandamizwa na dhulma, basi uwe ni ukumbusho kwa kila
yule ambaye ameitoa nafsi yake kwa ajili ya kuutumikia umma, asiizuwie
nafsi yake kutoa uhai wake pindi kunapokuwa na maslahi katika mazingira
yake.
Mwisho: Mimi nasema: "Ni mawaidha gani makubwa kuliko kufahamu kwamba,
kila aliyeshiriki kumwaga damu ya Husain a.s. tayari Mwenyezi Mungu
amekwishachukuwa kisasi chake, kwani huyo naye imma aliuawa au kufikwa
na msiba mkubwa. Au ni Mazingatio gani makubwa zaidi (yanatakiwa)
kuliko kuwa kaburi la Husain a.s ni eneo tukufu, wakati makaburi ya
maadui zake ni mahala pa kutupia vinyesi vya wanyama na mengine
yamefanywa kuwa machinjioni?
"Je waliofanya maovu wanadhani kuwa tutawafanya kama wale walio amini na
kutenda mema, ili kwamba uhai wao na mauti yao yawe sawa?
Ni hukumu mbaya kabisa wanayoihukumu" Qur'an 45:21
Kwa kumalizia naivamia meza ya washairi ili nisome beti kadhaa kutoka
ndani kabisa ya moyo wangu japo kwa ufupi ni msemeshe Imam huyu shujaa.
Ewe mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, utajo wako ni mzuri nawe
umetukuka mno kwa utajo huo na kwa fahari hiyo huna mfano wake.
Ewe Mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu moyo wangu umejaa utajo wako
Ni nani atakayeweza kudhibiti mambo yako mema, kwani kila jambo jema
hiyo ndiyo tabia yako ewe mwezi wenye nuru.
Ewe Mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mimi niko kwenye uongofu
aliotuongoza Ahmad Babu yako mwema.
Amani iwe juu yako asubuhi na jioni ulimwengu unakutakia, na wadudu pia
wanazisambaza salamu.
|