|
SHAHIDI WA KARBALA
SAYYIDINA IMAM HUSSEIN BIN ALI BIN ABI TALIB (A.S.)
Kimeandikwa Na: Sayyid Murtaza Rizvi
10 Muharram ni siku ya Ashura, Miaka 1364 iliyopita siku ambayo mjukuu
wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w.), Sayyidina Imam Hussein, mtoto wa Imam
Ali bin Abi Talib (a.s.) na mama Fatimah bint Muhammad (s.a.w.w.),
mrithi wa tatu wa haki wa Mtume wa Uislamu, mrithi wa Adam, Nuh,
Ibrahim, Musa, Isa, Muhammad na Ali, aliuliwa kikatili na Yazidi bin
Muawiyya bin Abu Sufyan baada ya kukataa kutoa kiapo cha utiifu kwa
Yazid.
Siku hii ni kumbu kumbu ya kujitoa muhanga kwa Imam Hussein (a.s.)
katika kuinususru Dini na kuitetea haki, dhidi ya wapinzani wa Uislam.
Sababu kubwa ya kuuliwa Imam Hussein ni kukataa dhuluma na uongo, na
kutaka kusimamisha Haki na Ukweli kama babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
alivyoamrisha. Tukio hili halikuwa la kawaida kwani Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
alishabashiri wakati aliposema: “Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam)
Hussein kitaamsha mori katika nyoyo za Waumini ambao hazitopoa milele.”
Rejea: (Mustadrak: J. 11, Uk. 27)
Siku hii, mamilioni wa Waumini Duniani kote wanaomboleza kifo cha Imam
Hussein (a.s.) kiigizo cha kweli cha Mtumishi wa Allah (s.w.t.)
muamarishaji nguvu za jeshi la Mungu dhidi ya majeshi ya Shetani,
tukiangalia historia ya Kiislam tunaona kuwa umma ulikwenda kinyume na
maamrisho na mafundisho ya Mtume (s.a.w.w.) ambayo alitaka tushikamane
nayo.
Imam Hussein alikuwa ni kizito cha pili kati ya vizito alivyotuamrisha
Mtume (s.a.w.w.) tushikamane navyo, kama Mtume mwenyewe alivyosema “Enyi
watu! Hakika mimi ninakuachieni vityu viwili vizito ambavyo mkishikamana
navyo hamtapotea milele, navyo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.)
Qur’ani na kizazi changu yaani Ahlul-Bayt (a.s.)”. Rejea: (Tirmiz-Juzuu
ya 5, Uk. 433. na Riyadhus-Salihiyn, Uk. 165, Babu Ikrami Ahlul-Bayt).
|